week1-lenten

 

Ukabila, Upendeleo wa Kiukoo na Siasa

Hapo kale, arusi kubwa ilifanyika angani na ndege wa aina mbali mbali wakaalikwa. Kobe alialikwa pia. Kabla ya kuanza safari ya kwenda angani, waliafikiana kuhusu kanuni za kuzingatiwa safarini na kwenye sherehe ya arusi. La muhimu zaidi kwenye makubaliano yao lilikuwa ni kugawana sawa kila kitu safarini na kwenye arusi. Walimteua Kobe kuwa kiongozi wao na kila ndege akampatia unyoya ili kumwezesha kupata mabawa ya kupaa juu. Ndege wote na rafiki yao Kobe walipaa kwenda arusi angani ambapo walikaribishwa na wenyeji wao. Kila mgeni aliombwa kujitambulisha. Ilipofika zamu ya Kobe, akafanya ujanja na kujibandika jina NINYI NYOTE.Wageni walipoletewa chakula, mhudumu alitangaza kuwa ni cha “ninyi nyote”. Vyote walivyoandaliwa wageni, iwe ni chakula, maziwa, matunda, mvinyo, vikatangazwa kuwa vya “Ninyi Nyote!”

Kobe alikula kwa pupa na kunywa vyote vilivyoandaliwa bila kuwajali marafiki wake. Ndege waliomwalika hawakula wala kunywa chochote kwani Kobe alivunja makusudi mkataba walioafikiana wakitoka ardhini. Ndege walikasirika na kushindwa kuuvumilia mchezo mbaya wa Kobe. Karibu kila ndege alimpokonya Kobe unyoya aliomwazima na kumwacha na manyoya machache tu ya marafiki zake wa karibu ambayo hayangetosha kumwezesha kuruka chini kurudi nyumbani.
Kobe alimtuma ndege mmoja rafikiye kwa mke wake ardhini akimwomba amwandalie godoro ili kumwezesha kutua salama. Lakini ndege aliyetumwa hakufikisha ujumbe kamili. Badala ya kumwandalia godoro,Bi Kobe alitandaza chini mawe yenye ncha kali, chupa zilizovunjika na vyuma vyenye makali. Kobe akapashwa habari kwamba kila kitu duniani kilikuwa shwari. Kuruka chini, alivunjika vipande.

Uchambuzi Kuamsha hisia za kikabila kwa manufaa ya kisiasa ya watu fulani binafsi ni mojawapo ya matatizo yanayokumba Kenya. Ili kuweza kutambua

vyema kiini cha ushindani uliopo sasa wa kisiasa unaoegemea ukabila, ubaguzi na dhuluma, tunahitaji kujiuliza maswali kadhaa. Pana uhusiano gani kati ya makundi yanayozingatia utamaduni fulani au hata makabila na mivutano ya ufuasi wa kisiasa na manufaa ya binafsi ya kisiasa? Tatizo la ukabila limekuwa na athari gani kwa maisha ya kila mtu na pia siasa za nchi? Je, Wakristo na wafuasi wa dini nyingine wamefaulu kuuweka mbali ukabila na uhasama ambao ovu hilo linazusha?
Katika kutafuta ufumbuzi wa masuala hayo, Kanisa linaomba kuwa msimu huu wa Kwaresima, watu wote wenye mapenzi mema, na hasa Wakristo Wakatoliki, waangazie masuala ya athari za ukabila ukitumiwa vibaya kwa usawa wa raia wote wa nchi, na hasa kuwatenga wengine kwa sababu ya asili zao za kikabila. Kadhalika, Kanisa Katoliki linafahamu kikamilifu kwamba pana tatizo la kushirikisha mila na tamaduni zetu mbali mbali katika taratibu za kutuunganisha kisiasa na pia kukuza demokrasia. Tatizo hilo huathiri dhana ya ujenzi wa nchi na taifa, uraia na manufaa ya wote katika jamii.
Kama tulivyosimuliwa katika hadithi ya kobe na ndege, Kenya ni taifa la watu wa makabila mbali mbali, na jamii tofauti zimeishi kwa amani na umoja kwa miaka mingi. Hali hii ya amani na utulivu miongoni mwa jamii mbali mbali imewezekana kwa sababu kila jamii ikizingatia tamaduni na mila zake imechangia katika kulijenga taifa la Kenya. Hata hivyo, bado tuna tatizo kubwa la kujenga nchi yetu kuwa taifa lenye kundi la watu lililotangamana na ambalo linajitambulisha kwanza kabisa kama Wakenya. Tukiweza kufikia hali hiyo ya kujiona kuwa Wakenya kwanza na wala si watu kutoka makabila mbali mbali, tutaweza kuzika tofauti zetu za kikabila na kidini na pia madhara yake. Utaifa na uzalendo sio tu kuwa katika maeneo jirani ama kupata kitambulisho cha uraia, lakini ni kutambua na kufahamu maadili ya kitaifa kama yalivyoelezwa katika Kifungu 10 (2) cha Katiba. Maadili ya kanuni za uongozi ni pamoja na:-

  • Uzalendo, umoja wa kitaifa, kushirikiana na ugatuzi wa mamlaka, utawala wa sheria, demokrasia na kushiriki kwa watu;
  • Heshima ya binadamu, usawa, haki za jamii, kushirikishwa, haki za binadamu, kutobagua na kulindwa kwa makundi yaliyotengwa;
  • Utawala mwema, uadilifu, uwazi na uwajibikaji; na
  • Maendeleo endelevu.
  • Ndiposa tunapaswa kujihadhari na njama za wanasiasa na viongozi

wengine wasiojali ambao huamsha hisia za kikabila na pia kuunga mkono makundi ya kikabila kwa lengo la kujifaidi kisiasa wao binafsi, kama vile kutwaa vyombo vya utawala wa nchi. Je, tunawezaje kulitatua tatizo hilo la matumizi mabaya ya ukabila na siasa za kikabila? Tatizo lililopo si la kuwepo kwa makabila, la hasha! Changa moto ni kushirikisha jamii zote nchini katika mahusiano ya kijamii na taratibu za kisiasa.

Juhudi za kuimarisha demokrasia haziwezi kufanikiwa bila kutilia maanani changamoto ya kushirikisha Wakenya wote katika taratibu za taifa. Mradi wowote, uwe wa kijamii, kiuchumi ama kidini ambao unahusu ushirikishwaji wa watu ni lazima utilie maanani tamaduni za maisha ya watu binafsi, wala sio kutegemea upendelevu na ubaguzi wa walio mamlakani. Taratibu za kujenga taasisi zinazozingatia demokrasia zitafua dafu msingi wake ukiwa ni watu wote katika kila eneo la nchi. Hatuna budi kuzishangilia jamii zetu tofauti kwa kuwakubali wengine nakutambua kwamba kila mtu ulimwenguni ana asili yake ya kijamii au hata kabila. Tusikubali ukabila utuletee maangamizi. Lazima pia tuzingatie ustahiki kwa kutilia maanani mchango ambao kila mtu binafsi anaweza kutoa, bila kutumia kabila au msimamo wa kisiasa kuwa kigezo muhimu.

Masomo

Mwanzo 9:8-15 1

Petro 3:18- 22

Mariko 1:12-15

Masomo ya leo yanatukumbusha kwamba Mungu ameweka mkataba nasi. Taifa letu ni safina mpya ambamo Mungu ameahidi kutuweka ili kutukinga kutokana na maovu yote. Alifanya hivyo kwa kumtuma mwanawe ambaye alitufanya tuwe wanawe Mungu. Wito tunaopewa leo ni kutubu kwa zile mara nyingi ambazo tumeutumia ukabila kuwabagua wengine badala ya kufurahia umoja tunaohimizwa kuujenga wa jamii zetu tofauti nchini. Lazima tuepukane na mshawasha wa kujiona kuwa sisi ni bora kuwaliko wengine. Tunawezaje kutekeleza mafunzo ya Kristo kuupiga vita ukabila unaoendeleza chuki?

TENDA

  1. Je, tunakumbana na ukabila kwa njia na sura zipi katika jamii zetu leo?
  2. Ugatuzi unachangiaje katika kuendeleza chuki za kikabila?
  3. Ni hatua gani tunachukua kuruhusu watu wa jamii nyingine kupata nafasi katika makundi yetu ya kikabila?
  4. Tukiwa Wakristo, tumepewa wito gani kuleta mabadiliko na kupunguza ukabila tukilitilia maanani neno la Mungu na maudhui ya msimu huu wa Kwaresima?

 

Comments are closed.